Ushairi: Bahari ya Maisha
Akili zangu
Zasimama ufuoni
Macho yake
Yakikagua bahari
Papa,mkali kama mauti
Anahangaisha samaki
Kwa ndaro na maringo
Daima akijigamba
Kwamba baharini
Haupo uwezo unaotisha
Wala tisho linalomweza
Wakati anaedelea kutiririka
Huku miongoni mwa samaki
Wingu zito huzuni
Lazidi uzani
Kama kwa sumaku
Samaki wanavutwa pamoja
Na nyuma ya ngao ya umoja
Wanaenda mwendo wa mbele
Wakiimba nyimbo zenye cheche
Kwa hasira zenye moto
Papa anaongeza ukali
Bali umati wa samaki
Haulegei muumano
Wala mwendo wa mbele
Kupungua kasi
Mashambulizi makali
Ewaa! Mashambulizi!
Kutoka pande milioni
Dhibi ya papa muuaji
Sasa baharini
Nyimbo za ufanisi
Zinapaa angani
Kama moshi wa unahi
Na kubusu masikio
Kama muziki wa nyonza.
MASWALI
- (a) Huu ni utungo wa aina gani? (alama 2)
- (b) Kwa kutoa mifano fafanua sifa zinazoufanya utungo huu kuwa shairi (alama 4)
- (c) Eleza mawazo ya mshairi katika shairi hili (alama 5)
- (d) Taja na ueleze mbinu tatu za kifasihi katika shairi hili (alama 6)
- (e) Eleza maana ya maneno yafuatayo kulingana na shairi (alama 3)
- (i)Ndaro
- (ii)Cheche
- (iii)Nyonza