Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali yanayofuata
KUPE NA KUNGUNI
KUPE: Uchokozi ni wa nini
Ewe ndugu mkunguni?
Tu pamoja mawindoni
Ya nini kunihaini?
Unyonyaji kunita?
KUNGUNI: Kupe usinilaumu
Sisi sote wanwa damu
Ela moja ufahamu
Pamoja hatutadumu
Mwisho utaangamia
KUPE: Uchongezi wako wewe
Tamaa yako mwenyewe
Wataka watu wajuwe
Mwisho sote tuuliwe
Na ukoo kupoteza.
KUNGUNI: Mimi hunwa nikaenda
Bali wewe unaganda
Hadi kuwapa vidonda
Ndipo tiba wameunda
Majosho kukuoshea.
KUPE: Japo mimi sikinai
Sitarajii uhai
Nitakwenda kwa mbuai
Walio hawatambui
Yao damu tajinwia
KUNGUNI: Kuna wanyama wa pembe
Wendapo wakukurumbe
Na wale wasio pembe
Meno,kwato,vyao vyembe
Mwilio kupasulia.
KUPE: Tajizika manyoyani
Ndani ndani turabuni
Ngozi na masikioni
Na kwengineko laini
Katu ha’tonifikia.
KUNGUNI: Nakwambia zindukana
Kuna madawa mwanana
Kuosha na kudungana
Uhai hutauona
Siambe sikukwambia
KUPE: Hapo hujasema kitu
Nami sitaacha katu
Kuna wanyama wa mwitu
Wasiofungwa na watu
Dawa hawatajitia
KUNGUNI: Kwa vile hujaghairi
Meshika yako hiari
Puuza langu shauri
Mwisho utatasawari
Hapo tungo naishia.
MASWALI
(a) Hili ni shairi la aina gani? (alama 2)
(b) Eleza maadhui ya shairi hili (alama 3)
(c) Bainisha sababu ya kutumiwa kwa maswali ya balagha (alama 2)
(d) Eleza umbo la shairi hili. (alama 4)
(e) Ni sababu gani inayoonyesha kuwa kunguni si mchochezi. (alama 2)
(f) Andika ubeti wa sita kwa lugha ya nathari. (alama 4)
(g) Eleza maana ya maneno (alama 3)
(i) majosho
(ii) uchongezi
(iii) mwanana
Your Reliable Homework Companion You Can Count On