SEHEMU YA A: USHAIRI
Ikilia ya mgambo, daima huwa na jambo,
Wa hapa na kule ng’ambo, ebu sikizeni mambo,
Mshikilie ya tambo, lisiwapige kikumbo,
Vipi mmekuwa nduli, kuhasiri kina mama?
Kuna wasasi haramu, waliojaa dhulumu,
Hawasaki nyama mwitu, windo lao mwanadamu,
Huvizia kina mama, kwa kigomba chenye sumu,
Jihadhari nao nduli, wasije wakakudhili.
Makucha yao makali, na magego yenye ncha,
Yamshinda homa kali, namna yanavyochukicha,
Hurarua kwa ukali, pasi hata kujificha,
Vipi mmekuwa nduli, kuhasiri kina mama?
Kwa uchu wanavamia, mithili ya nyama nofu,
Kila kiwakabilia, mnawanyofoa nyofu,
Redioni twasikia, umekuwa uzoefu,
Vipi mmekuwa nduli, kuhasiri kina mama?
Watenda uhayawani, utu kuubatilisha,
Husalia maskini, hondi yao kukatisha,
Ni mithili ya shetani, jambo hili linatisha,
Vipi mmekuwa nduli, kuhasiri kina mama?
Jamani unyama huu, haufai ni laana,
Mila wanazisahau, hawamtii Rabana,
Soteni washika dau, nduli tuanza sakana,
Vipi mmekuwa nduli, kuhasiri kina mama?
Inafaa kukomesha, kwa kuwatia mbaroni,
Wale wenye kupotosha, wapelekeni kortini,
Hata kitanzi zungusha, na mkikaze shingoni,
Vipi mmekuwa nduli, kuhasiri kina mama?
Sote na tujizatiti, ubakaji kuondoa,
Imara tuwe thabiti, kwa umoja hadi nia,
Wazee na mabanati, msije kulimatia,
Vipi mmekuwa nduli, kuhasiri kina mama?
MASWALI
a) Eleza ujumbe wa shairi hili (alama 4)b) Kwa mujibu wa shairi hili ni kina nani wanaomithilishwa na nduli (alama 2)
c) Eleza muundo wa shairi hili (alama 4)
d) Mshairi/mtunzi ametumia tamathali za usemi katika kila ubeti. Taja mbili kati yazo (alama 4)
e) Andika ubeti wa sita kwa lugha nathari (alama 4)
f) Huku ukitoa mifano eleza namna mshairi ametumia idhini yake (alama 4)